Maswali ya mara kwa mara

KWA NINI MWANACHAMA HASHIRIKISHWI KWENYE KWENYE MAAMUZI CHAMANI MFANO KUAMUA KIWANGO CHA KUCHANGIA AKIBA YA MWEZI?

JIBU: Kwa mujibu wa sheria za ushirika katika uendeshaji wa vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo kila mwanachama anayo haki sawa na mwanachama mwingine. Kila mwanachama anayo haki ya kutoa maoni yake katika vikao/ mikutano ya wanachama ngazi ya Wilaya, mkoa na hata mkutano mkuu. URA SACCOS Ltd katika ngazi ya Wilaya kuna Mwakilishi aliyechaguliwa na wanachama kwenye wilaya hiyo husika. Mwakilishi huyo ndiye anayewakilisha wanachama katika Mkutano Mkuu kwa kuwasilisha maoni ya wanachama wa Wilaya yake. Utaratibu huu umeainishwa katika sheria ya vyama vya Ushirika sehemu ya KF /42. Lakini pia kwenye jedwali la tatu 1(6) kimeruhusu uwakilishi kutokana na ukubwa na muundo wa chama.

KWA NINI MWANACHAMA AKIWA NA MKOPO HARUHUSIWI KUOMBA AKIBA YAKE ILI HALI MKOPO TAYARI UNA BIMA?

Akiba hizo ndo msingi mkubwa wa kupatikana kwa mikopo yetu. Changamoto kubwa ni kwamba wakati mwingine mkopo anaokopa mwanachama ni mkubwa sana kuliko akiba zake chamani. Kwa hali hiyo ni kwamba huo mkopo atakuwa amekopa na akiba zake za wenzake. Ili aweze kuomba akiba zake, hapo inamlazimu arudishe kwanza mkopo (Akiba alizokopa) ndo aombe akiba zake. Lakini pia mwanachama huyo anaruhusiwa kuomba kiasi cha akiba kinachozidi kiasi cha deni la mkopo analodaiwa.

KWA NINI MUDA WA MKOPO USIONGEZWE TOKA MIAKA 4 NA KUWA ZAIDI YA HAPO?

Kwa mujibu wa sheria ya Ushirika ukomo wa kutoa mkopo kwa nyama vya Ushirika ni miaka 5. Chama chetu kinatoa mikopo kwa miaka 4 bado nafasi ya mwaka mmoja tu ifikie kikomo. Uwezekano wa kuongeza muda inawezekana kama chama kina uwezo wa Ukwasi. Ikumbukwe kuwa mikopo hiyo kwa kiasi kikubwa hutokana na michango ya wanachama. Kama tukiongeza muda wa mkopo maana yake itaongeza mpaka kiasi cha kukopa. Kama kiasi cha kukopa kitaongezeka bila mkakati wa kuongeza michango basi mbeleni tunaweza kukwama kutoa huduma kwa wakati.

KWA NINI POSHO YA KIKAO HAITOLEWI TASLIMU?

Sababu  ya kutotoa posho ya kikao kwa mfumo wa taslimu kwa wanachama ni kutokana na changamoto kubwa ya ukwasi chamani.  Kwamba Demand ya huduma kwa wateja ni kubwa kuliko Supply ( nguvu ya kifedha) na utaratibu unaotumika ni kuiweka aidha kwenye akiba zake au hisa zake ili isaidie mzunguko wa kifedha kwa kutoa huduma chamani kuliko kuitoa kwenye mzunguko kwa kuilipa taslimu. Lakini pia hii ina tija zaidi kwa mwanachama kwani inaongeza thamani kwenye fedha zake kwa kuipata ile faida juu akiba zake au kupata faida juu ya hisa zake za hiari. Huo ni uwekezaji wake pia.

KWA NINI WAWAKILISHI WANATEULIWA NA WAKUU WA HIMAYA, BADALA YA KUCHAGULIWA NA WANACHAMA KWENYE HIMAYA?

Kwa mujibu wa sheria ya Ushirika Namba 6 ya mwaka 2013, Mwakilishi anatakiwa kuchaguliwa na wanachama kwenye himaya yake badala ya kuteuliwa na Mkuu au Mlezi wa chama kwenye himaya.

KWA NINI NIKIOMBA AKIBA ZANGU AIPEWI ZOTE, NA HATA NIKIPEWA KIASI SIZIPATI KWA WAKATI, MPAKA BAADA YA MIEZI 3?

Kwa mujibu wa sheria ya vyama vya Ushirika sehemu ya VII K/F 71(1) hairuhusiwi kwa mwanachama kuchukua sehemu ya akiba yake. Lakini kwa kizingatia kwamba wanachama wake wanaweka akiba kwa viwango na malengo tofauti tofauti, basi Ushirika ukaona ni busara aruhusiwe kuchukua sehemu ya akiba zake kwa kuacha 60% ya Akiba ya msingi na kuchukua 40% ya akiba ya msingi. Uombaji wa hiyo akiba utamlazimu atoe notisi ya angalau siku 90 ili akiba hiyo iandaliwe kwani fedha hizo ziko kwenye mzunguko ( zimekopwa).

MBONA HIYO FAIDA NA MAGAWIO HATUJAWAHI KUYAONA TANGU TUMEJIUNGA?

Gawio ni sehemu ya ziada inayopatikana baada ya hesabu za chama kukaguliwa na mkaguzi wa nje na kutoa matengo yote ya kisheria. Kinachobaki ndo gawio kwa wanahisa baada ya maamuzi ya Mkutano Mkuu kwa mujibu wa Masharti ya Chama sehemu ya 9 (c) na Kanuni ya Ushirika ya mwaka 2015 K/F cha 67 (d) . Mgao huo hufanywa kulingana na hisa anazomiliki mwanachama. Ikiwa chama kinataka kukuza mtaji au kuwekeza rasilimali, kiasi hicho cha mgao kitaongezwa kwenye hisa za mwanachama, yaani zitagawiwa hisa za bonus kwa kulingana na hisa alizonazo mwanachama. Hivyo basi chama kimekuwa kikitoa gawio kwa kila mwanahisa na kuziongeza katika akaunti ya hisa ya kila mwanachama kwa kila mwaka wa fedha wa chama baada ya hesabu za chama kukaguliwa na kuwasilishwa katika Mkutano Mkuu.

 

Faida juu ya akiba za mwanachama ni matumizi kutokana na bajeti ya mapato na matumizi ya mwaka husika. Faida hiyo ambayo kwa sasa ni 5.5% ya michango  yake (ambayo inaweza kubadilika mwaka wowote kwa maamuzi ya Mkutano Mkuu) anaipata mapema. Faida hiyo inawekwa moja kwa moja kwenye michango yake.