Habari zote

MATUKIO

URA SACCOS yakabidhi vifaa tiba vya TZS milioni 235.5 kwa Jeshi la Polisi

IGP Camillus Wambura amepokea mashine ya X-ray, vifaa vya maabara na vya wodini katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi la Polisi, Kilwa Road. Tangu 2017 chama kimetoa vifaa tiba vya zaidi ya TZS milioni 581.

URASACCOS Admin

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Camillus Wambura, tarehe 20 Aprili 2024 amepokea msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya TZS milioni 235.5 kutoka URA SACCOS Ltd katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi la Polisi iliyopo Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam. Msaada huo unajumuisha mashine ya X-ray ya kisasa, vifaa vya maabara, vifaa vya mazoezi tiba na vifaa vya wodini vya kulazia wagonjwa.

IGP Wambura amesema vifaa hivyo vimefika wakati muafaka ambapo Jeshi la Polisi lipo katika hatua mbalimbali za maboresho, ikiwemo kuhakikisha askari wanapata huduma bora za afya. "Vifaa tiba hivi vitaendelea kusaidia kupanua wigo wa utoaji huduma katika vituo tiba vyetu kwa watumishi wa Jeshi la Polisi, familia zao na wananchi kwa ujumla," alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya URA SACCOS Ltd, CP Suzan Kaganda, amesema chama kina utaratibu wa kutenga fedha kutoka kwenye ziada inayopatikana na kuirudisha kwa jamii kama msingi wa saba wa ushirika unavyotaka. Tangu utaratibu huo ulipoanza mwaka 2017, chama kimeshatoa kwa jamii vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya TZS milioni 581.

Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Anjela Nalimi, ameipongeza URA SACCOS na kusema iwe chachu kwa vyama vingine kuiga mfano huo. Vifaa hivyo vinatumika katika Hospitali ya Rufaa ya Kilwa Road na zahanati sita za Polisi: Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, Shule ya Polisi Moshi, na zahanati za Polisi mikoa ya Mtwara, Tanga, Dodoma na Kaskazini Pemba.

Picha zaidi

Imechapishwa pia kwenye Instagram

Shiriki:
URA SACCOS yakabidhi vifaa tiba vya TZS milioni 235.5 kwa Jeshi la Polisi | URASACCOS